Kitabu hiki kinachohusu ¿Usawiri wa Nyimbo za Magosi za Wanyakyusa katika Muktadha wa Tanzaniä kimechunguza historia ya uhusiano uliopo baina ya fasihi na jamii inayopigwa na wimbi la muktadha wa ulimwengu wa leo kupitia nyimo za Magosi za Wanyakyusa. Kitabu kinabainisha namna nyimbo teule zinavyosawiri hali halisi iliyopo nchini Tanzania kwa kurejelea muktadha mpana wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Kitabu hiki si tu kinahusu usawiri wa nyimbo za Magosi katika maendeleo ya Fasihi ya Kiswahili, bali pia ni chimbuko na historia, utamaduni, sheria na uhakimu, utawala, makazi na falsafa ya jamii ya Wanyakyusa. Historia ya maendeleo ya ushairi simulizi imeelezwa kwa undani ili kujenga mwega wa mjadala wa taarifa katika karne iliyopo sasa. Mwanazuoni anayetaka kuzama na kuchambua masuala muhimu yaliyomo katika kitabu hiki atakuwa amezima kiu yake baada ya kuchota kutoka kisima hiki chenye maji mengi na yaliyo salama. Kitabu hiki, kwa maana yake, kinahusishwa na Ujumi wa Mtu Mweusi kwa kuwa kinachochea mijadala ya masuala mengi yanayohusu historia, utamaduni wa Kiswahili na Kiafrika kwa wasomaji na watafiti wa sanaa za kijamii.